karibuni

chuki ikiingia ndani kupitia mlangoni upendo hutoka nje kupitia dirishani,upendo unagharama sana ukilinganisha na chuki,afadhali kununua upendo kuliko kuzawadiwa chuki na migogogro

February 08, 2008

HUYU NDIYE WAZIRI MKUU MPYA WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


Bunge nchini Tanzania limeidhinisha uteuzi wa Mizengo Kayanza Peter Pinda kuwa waziri mkuu mpya saa chache baada ya kupendekezwa na Rais Jakaya Kikwete.

Bwana Pinda ataapishwa na Rais Kikwete Jumamosi tarehe 9 katika ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Baraza jipya la mawaziri latarajiwa kuundwa hapo Jumatatu na mawaziri wapya kuapishwa Jumatano.

Uteuzi wa Bwana Pinda uliungwa mkono na wabunge 279. Alipingwa na wabunge wawili peke yake. Kura moja iliharibika.

Hadi kuteuliwa kwake, Bwana Pinda alikuwa waziri wa tawala za mikoa na serikali za mitaa.

Amekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi kwa muda mrefu na aliwahi kuhudumu kama msaidizi ikulu wakati wa uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Edward Lowassa

Hapo Alhamis Rais Jakaya Kikwete alivunja baraza lake la mawaziri baada ya kukubali kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Edward Lowassa.

Rais Kikwete pia aliitikia ombi la mawaziri wengine wawili ambao, pamoja na Bwana Lowassa, walihusishwa katika kashfa ya ubadhirifu na rushwa.

Rais Jakaya Kikwete
Rais Kikwete kumwapisha waziri mkuu mpya

Haijajulikana ni lini Rais Kikwete atamteua waziri mkuu mpya na kuunda baraza jipya la mawaziri.

Akitangaza hatua yake katika bunge Alhamis asubuhi, Bwana Lowassa alisema: "Nimetafakari sana kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya serikali yangu, nimeamua kumwandikia Rais barua ya kumuomba niachie ngazi."

Sakata hiyo inahusu zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond kuzalisha megawati 100 za umeme wa dharura.

Mawaziri wengine walioomba kujiuzulu ni Nazir Karamagi wa Nishati na Madini pamoja na mwenzake wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ibrahim Msabaha.

Uongo ndani ya bunge

Bwana Lowassa aliteta kwamba kamati teule ya bunge iliyomhusisha na kashfa ya Richmond ilimnyima haki ya kujieleza.

Alisema alikuwa ametafakari kwa makini kuhusu shutuma hizo na kufikia uamuzi kwamba, "tatizo ni uaziri mkuu."

"Kwamba ionenekane Waziri Mkuu ndiye amefanya haya, tumwondolee heshima au tumwajibishe."

Akielezea hatua yake ya kujiuzulu, Bwana Lowassa aliongeza "ninafanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa ili kuonyesha dhana ya uajibikaji na pia kutokukubaliana na utaratibu uliotumika kusema uongo ndani ya bunge kwa kumsingizia mtu."

Nguvu kubwa

Zabuni hiyo ilipewa kampuni ya Richmond Development group yenye makao yake nchini Marekani.

Kamati teule ya bunge kwenye ripoti yake iliyowasilishwa hapo Jumatano, ilipendekeza kujiuzulu au kuchukuliwa hatua kali kwa wahusika.

Waziri Mkuu akosolewa
Kutokana na ushahidi wa kimaandishi, kimazingira na wa kimdomo inaiona nguvu hiyo kuwa ni Waziri Mkuu
Kamati teule ya bunge

Ripoti hiyo iliwasilishwa bunge na Mwenyekiti wa kamati hiyo teule, Harrison Mwakyembe.

Kuhusu Waziri Mkuu, ripoti hiyo inasema: "Uamuzi wa serikali kuizuia Tanesco ( Shirika la umeme Tanzania) isivunje mkataba na kampuni hiyo licha ya sababu zote za kisheria kuwepo ni baadhi tu ya viashiria vya nguvu kubwa iliyojuu ya wizara ya nishati na madini."

"Kutokana na ushahidi wa kimaandishi, kimazingira na wa kimdomo inaiona nguvu hiyo kuwa ni Waziri Mkuu."

Kikatiba ndiye mwenye madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji na utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za serikali.

Yeye pia ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.

"Kamati teule haikufurahishwa hata kidogo na taarifa hizo zinazomgusa moja kwa moja Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kuipendelea Richmond."

Ubadhirifu na rushwa

Mawaziri wengine walioshutumiwa katika ripoti hiyo ni yule anayehusika na nishati na madini, Nazir Karamagi, mtangulizi wake Dr. Ibrahim Msabaha ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa takukuru, ilikuwa motoni kwa kutoa maelezo ya uongo kwa kamati hiyo.

Edward Lowassa
Aliteta kwamba hakutendewa haki na kamati ya bunge

Mbunge Mwakyembe alisema kamati yake ilitaka kuweka wazi kwamba mchakato wa zabuni ya kuzalisha nguvu za umeme kwa dharura wa megawati 100 ulighubikwa na vitendo vya ukiukwaji taratibu, kanuni na sheria za nchi."

"Na hivyo kujenga kiwingu cha mashaka ya upendeleo, ubadhirifu na rushwa ambavyo vimechangia kumwongezea mwananchi mzigo wa gharama za umeme."

Takukuru yashutumiwa

Taifa lilikuwa limetumbukizwa kwenye hasara kubwa kutokana na mkataba huo wa Richmond kinyume na taarifa iliyotolewa na Takukuru (taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa).

Uongo wa Richmond
Kwa nini kamati ya wataalamu haikuihoji Richmond kuhusu uongo huo bayana?
Kamati teule ya bunge

Ilishutumiwa kwa kujiharibia sifa yenyewe baada ya kutoa ushahidi wa uongo ikisema mchakato wa zabuni hiyo ulikuwa wazi, shirikishi na ulizingatia kanuni na kwamba dosari zilizojitokeza hazikuhitimu kuiletea taifa hasara.

"Taarifa hiyo imemong'onyoa kwa kiasi kikubwa hadhi na heshima ya chombo hiki muhimu cha kitaifa kilichopewa dhamana ya kupambana na rushwa na siyo kuipamba ili kurejesha heshima ya umma katika taasisi hiyo."

Ramani ya Tanzania
Richmond ilidai kuwa na miradi mikubwa Tanzania

Kamati hiyo ilipendekeza mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi hiyo.

Mbunge Harrison alisema kwenye tovuti yake, kampuni ya Richmond "ilikuwa inajitangaza kimataifa kipindi hicho kuwa kampuni yenye miradi mikubwa Tanzania ya ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha michezo, ujenzi wa bomba la mafuta la kilomita 1150 na ukarabati wa viwanja kadhaa vya ndege nchini."

Kamati teule ilishindwa kuelewa "kwa nini kamati ya wataalamu haikuihoji Richmond kuhusu uongo huo bayana ambao uliokuwa ushahidi wa kutosha kuipotezea sifa za kuwa mzabuni?"

No comments: